Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Tom Barrack, mjumbe maalumu wa Marekani nchini Syria, hivi karibuni katika mahojiano na jarida la National, alikiri kuwa Marekani imejaribu mara mbili hapo awali kuubadilisha (kuuangusha) utawala wa Iran, lakini juhudi hizo hazikufanikiwa kabisa. Alisisitiza kuwa sera hiyo imeshindwa na haipaswi kurudiwa tena.
Barrack alidai kuwa kubadilisha utawala wa Iran si sera ya sasa ya Marekani, na kwamba migogoro na Tehran inapaswa kutatuliwa kupitia mfumo wa kikanda na mazungumzo kati ya nchi jirani.
Vilevile alidai kuwa Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, yuko tayari kufanya mazungumzo ya kweli na Iran, lakini kwa sharti kwamba viongozi wa Iran waonyeshe “dhati” na kujitolea kushiriki kwa njia chanya.
Hata hivyo, kauli hizi zinakuja katika hali ambayo Trump mwenyewe aliwahi kukiri kuhusika katika kupanga na kusimamia mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya ardhi ya Iran, na mara kadhaa alijivunia mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran wakati wa mazungumzo.
Mkakati wa Shinikizo, Vikwazo na Kutarajia Maasi ya Wananchi
Katika muktadha huo, William O. Beeman, mwandishi, mtafiti wa Mashariki ya Kati na profesa wa Anthropology katika Chuo Kikuu cha Minnesota, alisema katika mahojiano na ABNA kwamba: “Katika mazingira ya sasa ya kisiasa, serikali ya Marekani chini ya Trump haitabadilisha sera yake ya kuitaka kuuangusha utawala wa Iran. Marekani ina historia ndefu ya kujaribu kufanya hivyo, licha ya sera hiyo kuonekana wazi kuwa imeshindwa.”
Beeman alieleza kuwa tangu enzi za urais wa George W. Bush, Marekani imeamini kuwa kwa kuiweka Iran katika vikwazo vya kiuchumi, kuitenga kimataifa na kuishambulia kwa vitisho, wananchi wake watafikia hatua ya kuasi na kuuangusha utawala wao. “Huu ni mkakati wa kipuuzi, lakini bado unaungwa mkono na wanahafidhina wakongwe (Neoconservatives) walioko serikalini na katika taasisi kama Taasisi ya Washington, American Enterprise Institute, na AIPAC.”
Aliongeza kuwa wakati mwingine Marekani imekuwa ikiunga mkono makundi ya upinzani kama Mujahideen Khalq (MEK) licha ya udhaifu wao mkubwa kisiasa.
Trump na Ndoto ya Tuzo ya Amani: Mazungumzo au Uporaji wa Kisiasa?
Akijibu swali kama kauli za Barrack zinaweza kuashiria matumaini ya kuboresha uhusiano wa Marekani na Iran, Beeman alisema: “Trump anatamani kujijengea sifa kama rais wa amani. Marais wawili wa Kidemokrasia – Jimmy Carter na Barack Obama – waliwahi kupata Tuzo ya Amani ya Nobel, na Trump anatamani kuipata pia. Lakini kwa bahati mbaya hana ujuzi wa diplomasia.”
Kwa mujibu wa Beeman, mtazamo wa Trump kuhusu amani unategemea kulazimisha mataifa, kuyabana na kuyanyanyasa ili yatii ajenda yake.
Kuhusu Iran, alisema Trump yuko tayari tu kwa mazungumzo endapo:
- Iran itasitisha kabisa maendeleo ya nishati ya nyuklia
- Vituo vyote vya nyuklia vibomolewe
- Jeshi la Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) livunjwe
- Iran isitishe kuunga mkono Hizbullah nchini Lebanon na Ansarullah (Houthis) nchini Yemen
Beeman alisisitiza: “Haya si mazungumzo ya amani; huu ni ubeberu wa kisiasa. Serikali ya Iran haitaikubali kamwe, kwa sababu matokeo yake ni kuporomoka kwa serikali na mabadiliko ya utawala kwa shinikizo la Marekani.”
Madai ya Kuachwa kwa Sera ya Kubadilisha Utawala ni Batili
Kuhusu madai ya Barrack kwamba kubadilisha utawala wa Iran si tena sera ya Marekani, Beeman alisema wazi: “Barrack anakosea. Bado kuna nia kubwa ya kuubadilisha utawala wa Iran, iwe rasmi au si rasmi.”
Alisema kuwa mazungumzo ya kikanda kuhusu usalama na rasilimali za pamoja, kama vile uwanja wa gesi wa Pars Kusini, ni hatua chanya, lakini: “Marekani chini ya Trump inataka uongozi wa sasa wa kisiasa nchini Iran ubadilishwe na kuwekwa viongozi wanaolingana zaidi na maslahi ya Marekani.”
Wapinzani wa Iran Ughaibuni na Siasa za Marekani
Beeman alifichua pia kwamba: “Baadhi ya Wairani wanaoishi nje ya nchi wanaounga mkono mabadiliko ya utawala walimpigia Trump kura mwaka 2016 na 2024 kwa matumaini kwamba atauangusha utawala wa Iran kisiasa au kijeshi.”
Kushindwa kwa Mara kwa Mara kwa Mkakati wa Marekani
Akizungumza kuhusu kushindwa kwa sera za kimarekani katika Iraq, Afghanistan na maeneo mengine, alisema: “Wazo kwamba unawaumiza wananchi ili waasi dhidi ya serikali yao ni mkakati uliotumiwa duniani kote – na haujawahi kufanikiwa kamwe.”
Beeman alihitimisha kwa kusema: “Mkakati huu umeshindwa kikamilifu na mara kwa mara. Hata hivyo, bado unaendelea kuwa msingi wa siasa za Marekani. Marekani imepoteza ushawishi wake katika kila nchi ilipojaribu kubadilisha utawala wake.”
Your Comment